Historia ya Somalia
Historia ya Somalia inahusu eneo la Afrika Mashariki ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Somalia.
Ukoloni wa Italia
Kuanzia mwaka 1888 Italia ilijipatia mikataba ya ulinzi na masultani mbalimbali waliotawala maeneo madogo kwenye Pembe ya Afrika. Walitangulia 1889 na sultani ya bandari ya Hobyo na mtawala wa usultani wa Majerteen.
Mwaka 1892 Usultani wa Zanzibar ulikodisha bandari ya Banadir kati ya Mogadishu hadi Brava kwa Italia. Mwaka 1905 Italia ilinunua eneo hili kutoka Zanzibar na kulitangaza kuwa koloni na Mogadishu kuwa mji mkuu.
Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Waitalia walikabidhiwa na Uingereza eneo la Kismayu. Walilitawala kwa jina la "Oltre Giuba" (ng'ambo ya mto Juba) na kuliunganisha na Somalia ya Kiitalia tarehe 30 Juni 1926.
Wakati uleule waliamua kumaliza hali ya sultani za Majarteen na Hobyo kuwa nchi lindwa na kuzifanya sehemu kamili za koloni. Mipango hiyo ilisababisha vita kali ya miaka miwili kwa sababu masultani waliona mikataba yao ya ulinzi ilivunjwa wakapinga jeshi la Italia.
Mwaka 1936 Somalia ikaunganishwa na Ethiopia kuwa sehemu ya Afrika ya Mashariki ya Kiitalia.
Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia makoloni ya Italia yalivamiwa na Uingereza uliotawala Somalia tangu 1941.
Mwaka 1949 Somalia ilirudishwa mikononi mwa Italia ilisimamie kwa niaba ya Umoja wa Mataifa.
Ukoloni wa Uingereza
Uingereza uliingia katika eneo hili baada ya Misri kuondoka mwaka 1885 kwa kushindwa na jeshi la Mahdi huko Sudan. Uingereza uliingia kwa sababu iliona umuhimu wa kutawala pande zote mbili za Bab el Mandeb ikihofia uenezaji wa nchi nyingine za Ulaya, hasa Ufaransa iliyokuwa na koloni la kwanza ya Ubuk (Obok) katika Jibuti ya leo tangu 1862. Pamoja na hayo Waingereza walitegemea kununua nyama kwa ajili ya mji wa Aden na meli zilizopita hapo kati ya Uhindi na Ulaya.
Somaliland ilitawaliwa awali kama mkoa wa Uhindi wa Kiingereza ikawa baadaye chini ya wizara ya makoloni huko London.
Hata kama Uingereza haukuwa na nia ya kuingilia mno maisha ya wenyeji ulikutana na upinzani mkali kuanzia mwaka 1899 kutoka kwa kiongozi wa dini Diiriye Guure, aliyeitwa na Waingereza "Mullah majununi". Waingereza walijibu kwa ukatili katika vita vya miaka 20 iliyoua takriban theluthi moja ya wakazi wote wa eneo.
Mwishowe Uingereza iliweza kumaliza upinzani kwa teknolojia mpya ya eropleni za kijeshi zilizotumia mabomu na bunduki za mtombo kutoka angani kwa mara ya kwanza katika Afrika.
Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia eneo likatwaliwa na Italia katika Agosti 1940 lakini lilichukuliwa tena na Uingereza katika Machi 1941.
Uhuru
Mwaka 1960 utawala wa kikoloni ulikwisha na Somalia ikapata uhuru wake, ikiunganisha makoloni mawiliː la Waitalia (kusini) na la Waingereza (kaskazini).
Baada ya mwaka 1991 nchi ya Somalia ilibaki haina serikali wala umoja wa taifa, bali iligawiwa na wakereketwa na wanamgambo wa ukoo na eneo, hasa Somaliland, Puntland na Galmudug upande wa kaskazini.
Katika miaka 2008-2013 ilihesabika kama nchi filisika. Kwa sasa ni nchi dhaifu lakini inaanza kujengwa upya kama shirikisho na kujiandaa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tarehe 4 Machi 2024 imejiunga rasmi na Jumuia ya Afrika Mashariki[1].
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Somalia kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |