Historia ya Angola
Historia ya Angola inahusu eneo la Kusini mwa Afrika ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Angola.
Wakazi wa kwanza huaminiwa kuwa wawindaji-wakusanyaji wa jamii ya Wasani.
Katika karne za kwanza BK walifika wahamiaji Wabantu wenye ujuzi wa kilimo na uhunzi.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Kuanzia karne ya 14, falme mbalimbali zilienea sehemu za Angola, kwa mfano Dola la Kongo, Dola la Lunda na Dola la Kasanje.
Dola la Kongo
[hariri | hariri chanzo]Ufalme wa Kongo ulikuwa dola lililoenea ndani ya nchi za leo za Angola, Kongo (Kinshasa) na Kongo (Brazzaville).
Ulianzishwa katika karne ya 14 ikadumu hadi karne ya 17.
Mtawala wake alikuwa na cheo cha "Mwene Kongo" au "Manikongo" wa kabila la Bakongo.
Ufalme huo umejulikana zaidi kihistoria kwa sababu ya mawasiliano yake ya kimataifa. Katika karne ya 15 meli za Wareno zilifika mwambaoni mwake.
Wakati wa kukutana na Wareno Ufalme wa Kongo labda ulikuwa na eneo la km² 300,000 ukaunganisha robo ya magharibi ya Kongo (Kinshasa) pamoja na sehemu za Angola na Kongo (Brazzaville).
Manikongo mbalimbali walijenga uhusiano na Ureno na Kongo ilikuwa taifa la kushikamana na Ureno hadi kuharibika kwa uhusiano huo. Katika kipindi kile taarifa mbalimbali ziliandikwa zinazotupa leo picha nzuri ya ufalme huo.
Manikongo alikaa katika mji wa M'banza-Kongo.
Baada ya wafalme kuwa Wakristo Wakatoliki na kujengwa kwa kanisa kuu, jina la "São Salvador do Congo" (kwa Kireno: "Mwokozi Mtakatifu wa Kongo") lilikuwa kawaida kwa mji mkuu wa milki.
Ufalme ukawa na majimbo, wilaya na vijiji. Majimbo yalikuwa saba ya Mpemba, Nsundi, Mpangu, Mbata, Mbamba na Soyo.
Kwa mikataba ya baadaye falme za Kakongo, Loango na Ngoy likatokea shirikisho ya sehemu nne.
Dola la Lunda
[hariri | hariri chanzo]Dola la Lunda lilikuwa ufalme wa Kibantu katika miaka 1600 hadi 1850 hivi kandoni kwa mto Kasai, mpakani kwa nchi za kisasa za Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Dola la Kasanje
[hariri | hariri chanzo]Dola la Kasanje lilikuwa ufalme wa Kibantu katika miaka 1620 hadi 1910 hivi kandoni kwa mto Kwango, upande wa kaskazini wa nchi ya kisasa ya Angola. Lilianzishwa na viongozi kutoka Dola la Lunda.
Mwaka 1910 lilivamiwa na Wareno na kuingizwa katika koloni lao la Angola.
Dola la Ndongo
[hariri | hariri chanzo]Dola lingine la kusini lilikuwa lile la Ndongo, lililopambana na Wareno miaka 30 chini ya malkia Njinga katika karne ya 17.
Vita vya uhuru
[hariri | hariri chanzo]Mwaka 1966 Jonas Savimbi alianzisha tapo la UNITA (kwa Kireno: União Nacional para a Independência Total de Angola) kama harakati ya kukomboa Angola kutoka ukoloni wa Ureno. UNITA ilikuwa moja kati ya harakati tatu zilizoshindana.
UNITA ilianza kama kikundi cha kikomunisti kufuatana na itikadi ya Mao Zedong. Uadui kati ya Wakomunisti wa Uchina na Urusi ulionekana katika mashindano ya UNITA dhidi ya MPLA (kwa Kireno: Movimento Popular de Libertação de Angola - Partido do Trabalho) iliyosaidiwa na Urusi.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe
[hariri | hariri chanzo]Baada ya uhuru mwaka 1975 MPLA ilitawala mji mkuu na kuunda serikali rasmi lakini Savimbi aliendelea kuipinga.
Savimbi alipata kupokea baadaye usaidizi kutoka maadui wote wa MPLA bila kujali itikadi. UNITA ilipata misaada toka serikali mbalimbali duniani ili kuiondoa madarakani serikali ya MPLA. Savimbi alikuwa akipata misaada ya fedha na silaha toka serikali za Marekani, China, Afrika Kusini, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (wakati huo ikijulikana kama Zaire), Moroko, n.k. Serikali ya Angola ilikuwa ikipata misaada toka Urusi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani, Kuba, na Nicaragua.
Tarehe 22 Machi 2002, Jonas Savimbi aliuawa vitani. Muda mfupi baadaye UNITA na MPLA zilikubaliana kusimamisha mapigano. UNITA ilichukua nafasi ya chama cha upinzani. Hata hivyo taratibu za kidemokrasia zilichelewa hadi chaguzi za miaka 2008 na 2012 na toleo la katiba mpya la mwaka 2010.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Angola kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |