Nenda kwa yaliyomo

Immanuel Kant

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Immanuel Kant
Taswira ya Immanuel Kant
Taswira ya Immanuel Kant
Alizaliwa 22 Aprili 1704
Alikufa 12 Februari 1804
Nchi Prussia (Ujerumani)
Kazi yake profesa wa chuo kikuu
mwanafalsafa

Immanuel Kant (22 Aprili 1704 - 12 Februari 1804) alikuwa mwanafalsafa Mjerumani kutoka milki ya Prussia. Anahesabiwa kati ya wanafalsafa muhimu zaidi wa Zama za Mwangaza.

Kant alizaliwa mjini Königsberg (sasa: Kaliningrad) kama mtoto wa fundi. Mama yake alimsomesha kweye shule ya sekondari akaendelea kusoma teolojia, falsafa, sayansi, fizikia na hisabati. Tasnifu (thesis) yake ya kwanza haikupokewa na profesa wake mwaka 1746, hivyo alifanya kazi ya mwalimu kwenye nyumba ya matajiri na makabaila mbalimbali kwenye mazingira ya Königsberg.

Mwaka 1754 alirudi chuo kikuu akamaliza masomo yake. Tangu mwaka 1755 alikuwa mwalimu na tangu 1770 profesa kamili kwenye chuo kikuu cha Königsberg.

Hakuoa; aliishi na mtumishi wa nyumbani tu hadi kifo chake mwaka 1804 kwa umri wa miaka 80. Kaburi lake liko kando ya kanisa kuu la Königsberg na limetunzwa hata siku hizi baada ya kufukuzwa kwa Wajerumani na kuwa sehemu ya Urusi.

Mwanafalsafa wa mwangaza

[hariri | hariri chanzo]

Kwa Kant kazi ya akili inaanza kwa kufikiri mwenyewe. Alisema: "Sapere aude!", na hii inamaanisha: "Usiogope kutafakari mwenyewe". Aliona ni muhimu kila mtu atumie akili yake mwenyewe badala ya kutegemea mawazo ya wengine. Mawazo na mafundisho yote yanapaswa kupitia kwenye uhakiki wa akili.

Kwa njia hiyo alitafsiri mwelekeo wa zama za mwangaza na wengi wanamwona kuwa alikamilisha jitihada za mwangaza. Kant aliandika: "Mwangaza unamaanisha kuondoka kwa binadamu kutoka uchanga wake uliosababisha mwenyewe. Uchanga unamaanisha kutotumia akili bila mwongozo wa mwingine. Uchanga huo husababishwa na mtu mwenyewe si kwa sababu ya uhaba wa akili lakini kwa sababu ya uhaba wa nia na hofu ya kutumia akili bila mwongozo wa mwingine."

Ngazi ya urazini

[hariri | hariri chanzo]

Katika kutafakari kwake Kant alipita njia. Mara nyingi hii inagawiwa katika vipindi viwili: kabla ya "uhakiki" na baada ya "uhakiki"". Tangu kutunga kitabu chake "Uhakiki wa akili tupu" alifundisha tofauti kuliko awali. Katika kipindi cha kwanza hadi 1760 alifuata mtindo wa walimu wake ulioitwa urazini (rationalism). Alirudia jinsi alivyofundishwa na wanafalsafa kama Leibnitz ya kwamba akili inaweza kutambua kila kitu.

Ngazi ya Uhakiki

[hariri | hariri chanzo]

Katika tasnifu yake alianza kusogea mbali na urazini unaofundisha kwamba akili inaweza kutambua ulimwengu na hali halisi ya vitu vyote. Kant alisisitiza ya kwamba si akili peke yake lakini pia maarifa na ufahamu. Kuona ni muhimu kama kutafakari.

Kazi ya falsafa aliona katika kufikiria uhusiano wa yale yanayopatikana akilini kama dhana na yale yanayonekana hali halisi katika mazingira ya mtu. Msingi huo ulikuwa mpya ukalazimisha kutafakari upya masuala mengi katika falsafa, hasa metafizikia.

Baada ya kupokea wito wa kuwa profesa Kant alikuwa na kipindi nyamavu cha miaka 10, maana yake alifundisha wanafunzi wake lakini hakutoa kitabu kipya, akitafakari yale yanayotokana na msingi wake mpya.

Alihitaji kulijibu swali: jinsi gani binadamu anapata ujuzi wake na jinsi gani akili inaweza kuushughulikia.

Maswali 4 ya Kant

[hariri | hariri chanzo]

Kant alijiuliza maswali manne:

  1. Ninaweza kujua nini?
  2. Ninatakiwa kufanya nini?
  3. Ninweza kutumaini nini?
  4. Binadamu ni nini?

Uhakiki wa akili tupu

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1771 alitoa kitabu "Uhakiki wa akili tupu". Humo aliuliza swali: akili inaweza kujua nini bila maarifa?

Anaangalia ujuzi wa "a priori" (Kilatini: kutoka chanzo). Kuna mambo ambayo tunayajua bila maarifa na ujuzi huo ni msingi wa kupata maarifa. Tunajua kuwepo kwa wakati na mahali bila kuviona - na kwa ujuzi huo ndani yetu hatuwezi kuelewa wakati fulani au mahali fulani. Hapa anaita hisabati aina ya "sayansi a priori" kwa sababu dhana zote za hisabati ziko bila maarifa yoyote.

Halafu anatazama mipaka ya akili. Akili inataka kuendelea lakini inagonga mipaka. Maswali kama: Je kuna roho ndani ya mtu isiyokufa? Kuna Mungu? Ulimwengu hauna mipaka? yanahusu mambo ambayo akili haiwezi kujibu kwa uhakika. Hakuna uthibitisho kwa namna ya kisayansi.

Uhakiki wa akili tendaji

[hariri | hariri chanzo]

"Uhakiki wa akili tendaji" ni kitabu cha pili kinachoendeleza kile cha kwanza. Akili tendaji ni matumizi ya akili kwa maadili ya kutenda yale ambayo ni mema na sahihi.

Hapa anafundisha "amri halisi": "Katika matendo yako fuata shabaha zile tu zinazofaa kuwa msingi wa sheria kwa watu wote."

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]
WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu: