Pieter Dirkszoon Keyser
Pieter Dirkszoon Keyser (aliyeitwa pia Petrus Theodorus; Emden, Ujerumani, 1540; Java, Indonesia ya leo, 11 Septemba 1596) alikuwa baharia katika utumishi wa Shirika ya Kiholanzi kwa Uhindi ya Mashariki (kwa Kiingereza Dutch East India Company).
Alifundishwa na Petrus Plancius elimu ya nyota na uchoraji wa ramani ya nyota.
Mwaka 1595 alikuwa nahodha wa safari ya kwanza ya Waholanzi kuelekea "Uhindi ya Mashariki", yaani visiwa vya Indonesia. Katika safari hii alichora ramani za nyota za nusutufe ya kusini, ambazo kwa jumla hazikujulikana bado huko Ulaya, na kubuni kundinyota mpya 12 [1].
Keyser alifariki kwenye safari hii mwaka 1596. Mwakilishi wa shirika Frederick de Houtman alirudi na ramani zake Uholanzi na kuzikabidhi kwa Plancius aliyezitumia katika globu ya nyota ya mwaka 1598.
Alitaja kama makundinyota mapya kwa Kiholanzi[2]:
- Het Chameljoen (Chamaeleon au Kinyonga)
- Den Dorado (Dorado au Panji)
- Den voghel Fenicx (Phoenix yaani finiksi au Zoraki)
- De Indiaen (Indian au Mhindi)
- Den Indiaenschen Exster, op Indies Lang ghenaemt („Kinubi cha Kihindi“) yaani Tucana au Tukani
- De Paradijs Voghel (Apus au Ndege wa Peponi)
- De Pauww (Pavo au Tausi)
- Den Reygher (Grus au Kuruki)
- De Waterslang (Hydrus au Nyoka Maji)
- De Vlieghe (Musca au Nzi)
- De vlieghende Visch (Volans au Panzimaji)
- Den Zuyder Trianghel (Triangulum Australe au Pembetatu ya Kusini)
Baada ya kuonekana kwenye atlasi ya Plancius majina haya yalichapishwa katika taarifa ya Frederick de Houtman kuhusu safari yake na mwaka 1603 katika "Uranometria", atlasi ya nyota iliyotolewa na Johann Bayer iliyoendelea kuwa msingi wa utaratibu wa kutaja nyota unaotumiwa hadi leo.
Makundinyota yake yamepokewa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia kati ya makundinyota rasmi zinazotumika leo hii kimataifa[3].
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Knobel, E. B. On Frederick de Houtman's catalogue of southern stars, and the origin of the southern constellations, Monthly Notices of the Royal Astronomical Society, Vol. 77, p.414-432, (March 1917). Tovuti ya harvard.edu, iliangaliwa Oktoba 2017
- ↑ Scouting the southern sky, Str TAles 1, tovuti Star Tales ya Ian Ridpath, iliangaliwa Oktoba 2017
- ↑ The constellations, tovuti ya Ukia, iliangaliwa Oktoba 2017